Na:Ayoub Mwigune na Halima Katala

Afisa michezo mkoa wa morogoro Neema Msithar  ameupongeza uongozi wa shule ya St.Marys mkoani Morogoro kwa kuwa na utaratibu wa kuandaa siku ya michezo ambayo inawashirikisha wazazi pamoja na walimu kwani siku hiyo imekuwa ni nyenzo ya kujenga uhusiano mzuri kati ya walimu pamoja na wazazi .

Akizungumza kwa niaba ya Afisa huyo wa michezo   mkoa, Afisa elimu wa manispaa ya Morogoro  bi. Imakulata Fungo alisema kuwa michezo inatakiwa ipewe kipaumbele kwani inachangia sana katika kuufanya mwili  uwe na afya njema na kuongeza uwezo wa kufikiri pia aliomba walimu wa michezo kuendelea kuwafundisha watoto michezo mbalimbali kwani kufanya hivyo kutawajengea wanafunzi hali ya kupenda shule.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo bi Jane Akisa   alitoa shukrani  kwa wazazi waliojitokeza katika siku hiyo ya michezo ambayo ilifanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na alisema  lengo la michezo hiyo ni kuwajenga wanafunzi ili kupenda michezo.

Michezo iliyochezwa ni pamoja na riadha ya mita 25 na mita 75 ,kula ndizi,kuokota viazi huku mchezo uliowasissimua wengi ni mchezo wa kuvuta kamba kati ya walimu na wazazi ambapo katika mchezo huo wa kuvuta kamba kati ya walimu wakiume na wazazi wakiume ilishuhudiwa wazazi wakiume wakiweza kuibuka washindi  kwa upande mwingine wazazi wakike waliweza kuzidiwa nguvu na  kupoteza ushindi dhidi ya walimu wakike .

 

Zawadi mbalimbali vikiwemo vikombe ziliweza kutolewa kwa vikundi pamoja na watu waliofanya vyema katika mashindano hayo.

TOA MAONI YAKO HAPA