Tamko hili lilitolewa na aliyekuwa waziri Mkuu wa Ghana Kwame Nkrumah mwaka 1967 katika andiko lake linalozungumzia mapitio ya siasa za kijamaa za kiafrika, nimeanza na andiko hili kuonyesha umuhimu wa kuzingatia usawa na misingi ambayo imejegwa katika kulinda haki za binadamu.

Tarehe 25 oktoba mwaka huu Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wake wa 5 unaoshirikisha vyama vingi, ikumbukwe kuwa uchaguzi wa mwaka 1995 uliomuingiza Rais Benjamini Mkapa madarakani ulikuwa uchaguzi wa kwanza na baada ya kumaliza vipindi vyake viwili na baada ya hapo akaingia Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 naye akakaa vipindi viwili na sasa muda wake unakwisha tunatarajia kuingia katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Pamoja na kufanyika kwa chaguzi nne sasa tangia kuwepo kwa vyama vingi, mara zote tumeshuhudia uchaguzi huru na wa amani japo kuna wakati kumekuwa na kasoro ndogondogo ambazo hata hivyo zilimalizwa kwa majadiliano katika meza ya duara japo zingine zimemalizwa na vyombo vinavyosimamia haki kama Mahakama.

Nimeona nizungumzie umuhimu wa amani katika uchaguzi huu ambao tofauti na chaguzi zingine ni uchaguzi ambao umekuwa na msisimko mkubwa na kuamsha hamasa kwa chama tawala na hata kwa upinzani.

Uchaguzi huu umechagizwa kwa kiasi kikubwa na chaguo la Chama cha Mapinduzi CCM yaani Mh. Dk John Pombe Magufuli na mpinzani wake katika uchaguzi huu ambaye pia alikuwa kada mkubwa wa chama hicho na Waziri Mkuu wa Zamani kabla ya kujiengua na kujiunga na chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema ambaye pia anaungwa mkono na vyama vilivyounda umoja wao maarufu kama Ukawa yenye vyama vya CUF, NCCR MAGEUZI NA NLD Mh. Edward Ngoyai Lowassa.

Uchaguzi wa mara hii unaonekana kuwa mgumu na kila chama kimeendelea kutamba kuwa kitashinda na hapa ndipo ninaposimamia katika hoja yangu ya kutaka kuwepo kwa amani katika uchaguzi wa mwaka huu kwa kile alichowahi kusema Waziri Mkuu wa zamani wa Ghana Kwame Nkrumah kwamba  kutokana na hali ya ubinadamu tuliyonayo lazime utoke katika misingi ya uchaguzi wa sera, kulinda na kudumisha usawa na haki za kibinadamu na hapo ndipo amani ya kweli itaendelea kudumu.

Sina maana kuwa natia mashaka katika wasimamizi wa Uchaguzi katika ngazi zote yaani tume ya Uchaguzi, ofisi ya Msimamizi wa Vyama ama taasisi nyingine yoyote ili, hapana nasisitiza kuwepo kwa uwazi na kuondoa aina yoyote ya mashaka ili kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi huru na wa amani.

Niliwahi kusoma andiko la filosofa mmoja maarufu Duniani  Lenin “Vita na Ujamaa” Lenin anasema “tunatambua vita vya wenyewe kwa wenyewe vya aina ya, vita vinavyotekelezwa na daraja la watu wanaokandamizwa dhidi ya wakandamizaji, watumwa dhidi ya wamiliki wa watumwa, vibarua dhidi ya wanaohodhi ardhi  na wafanyakazi dhidi ya mabwanyenye, kuwa vita hivi ni halali kabisa.”

Lenin anaonyesha kuwa mara nyingi vita hutokea pale watu wanapoamni kuwa kwa njia moja au nyingi wamekandamizwa na wakati mwingine kuwepo kwa uchochezi kutokana na hali hiyo ndipo unapoona umuhimu wa kuepuka aina yoyote ya ukandamizaji na uchochezi.

Kutokana na hali hii mimi binafsi naona mwanga wa amani kupitia tume yetu ya taifa ya uchaguzi chini ya Jaji Damian Lubuva katika mkutano wake na viongozi wa vyama vya siasa Lubuva amesisitiza kuwa tume yake ni huru na itatenda haki.

 “…..Ni kwamba kwenye katiba tume inafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yoyote yule hata Raisi haingilii utendaji wa tume” anasema Jaji Damiani Lubuva Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi.

Maneno hayo ya Jaji Lubuva yananifariji sana kuwa uchaguzi huu una kila sababu ya kuaminika na kuwa utakuwa uchaguzi wa kihistoria japo sisemi chaguzi zingine hazikuwa za kihistoria.

Mbali na Jaji Lubuva lakini pia nimefarijika na maneno ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Fransis Mutungi amewaambia wana habari kuwa serikali haiwezi kufumbia macho matendo ya uvunjifu wa amani ambayo yamejitokeza tangia kampeni za uchaguzi mwaka huu zizinduliwe.

“tusiende nyuma ya mgongo wa kisiasa tukatenda matendo ya kihalifu” anasema Jaji Mutungi.

Nahitimisha kwa kusema tujitokeze kwa wingi na kadi zetu za kupigia kura tarehe 25 octoba tukapige kura na tuhakikishe tunapiga kura kwa amani bila kutenda makosa ya jinai, tukumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na utamuangaliaje mtu uliyemtendea jinai.

Pia vyombo husika hakikisheni uchaguzi unakuwa huru na haki ili kuepusha uvunjifu wa amani na kisha kupelekwa kwenye mahakama ya kimataifa huko The HAGUE.

 

TOA MAONI YAKO HAPA