WEKENI MIPANGO YA MATUMIZI ENDELEVU YA ARDHI - WARIOBA

Na, Catherine Mangula Ogessa

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba  amekitaka chuo hicho kuhakikisha kinaweka mipaka katika maeneo yote ya ardhi ya chuo pindi mgogoro uliopo kati ya wananchi na SUA utakapomalizika, pamoja na kuwa na mpango endelevu wa matumizi ya ardhi.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba akiongea na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.(Picha na Fransis Mwakatenya)

 

Akizungumza na viongozi wa chuo hicho mara baada ya ziara yake ya siku mbili, iliyokuwa na lengo la kujifunza na kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho, Mkuu huyo wa chuo amesema, pamoja na kuwepo kwa uhaba wa fedha lakini ni muhimu kuhakikisha mipaka ya chuo  inakuwa wazi na kulindwa jambo litakalosaidia wananchi kuelewa na kutoingia katika maeneo ya chuo

 

Aidha Mhe. Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu katika awamu ya kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere amesema kuwepo kwa mpango wa matumizi ya ardhi pia kutasaidia kuhakikisha  maeneo hayo hayachukuliwi kwa matumizi mengine na badala yake yatumike kwa shughuli za chuo ikizingatiwa hivi sasa mji wa Morogoro unazidi kupanuka.

Jaji Mkuu (mstaafu), Mhe. Mohamed Chande Othman akiongea na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.(Picha na Fransis Mwakatenya)

 

Katika hatua nyingine amewapongeza viongozi  kwa jitihada wanazozifanya katika kuhakikisha wanamaliza changamoto za miundombinu na hatimaye wanafunzi waweze kusoma wakiwa katika mazingira rafiki, lakini pia kwa namna wafanyakazi wanataaluma pamoja na waendeshaji jinsi ambavyo wamekuwa wakitoa maelezo ya shughuli mbalimbali wanazozifanya  kwa kujiamini wakati wa ziara yake, hali inayoonesha wanaelewa kile wanachokifanya.

Amebainisha pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali lakini pia wamejitahidi kuhakikisha wanawaandaa wahitimu ili pindi wanapomaliza masomo yao waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine. Pia ameutaka uongozi huo kuhakikisha unaweka mikakati ya kuzidi kuongeza madarasa na maabara za kufundishia kwani pamoja na jitihada nzuri wanazozifanya za kuongeza madarasa na maabara lakini bado hazitoshi kwa siku za usoni kutokana na kuongezeka kwa udahili kila mwaka.

 

Awali akimkaribisha mkuu wa chuo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Jaji mkuu Mstaafu  Mh Mohamed Othuman Chande amekitaka chuo kuhakikisha kinashirikiana na Serikali ili kuwa na mtazamo mmoja katika mageuzi mbalimbali yanayofanywa chuoni hapo huku akisisitiza kuhakikisha chuo kinabaki katika malengo yake makuu ya kutoa mafunzo, utafiti na kutoa huduma kama vile ugani.

 

Akitoa shukrani kwa ujio wa Mkuu huyo wa Chuo, Naibu wa Makamu  wa Mkuu wa Chuo Taaluma Prof. Peter Gillah amesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote  hususani suala la kuweka mipaka ya ardhi pamoja na kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na yale yaliyoagizwa na mwenyekiti wa Baraza.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner