Serikali imeitaka tume ya Madini kuhakikisha inavuka lengo la kukusanya mapato kutoka shilingi Bilioni 310 hadi Bilioni 500

Na:Gerald Lwomile

Serikali imeiagiza Tume ya Madini nchini kuhakikisha inawatafuta wachimbaji wote wa madini ambao wamechelewa au hawataki kulipa madeni yao kutokana na mirahaba na wakithibitika kukwepa basi wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko wakati akifungua mafunzo ya namna bora za kukusanya mapato ya Serikali kwa wahasibu wa Wizara ya Madini waliotoka sehemu mbalimbali nchini.

Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko akifungua mafunzo ya namna bora za kukusanya mapato ya Serikali kwa wahasibu wa Wizara ya Madini waliotoka sehemu mbalimbali nchini uzinduzi huo uliofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Kampasi ya Solmon Mahlangu Morogoro.

Mhe. Biteko amesema, inashangaza kuona wachimbaji wadogo wanapopata maeneo ya kuchimba madini hunyang’anywa maeneo hayo na kupewa wachimbaji wakubwa ambao wana madeni mengi na hawajalipa madeni yao kwa muda mrefu

 Wahasibu wa Wizara ya Madini kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiwa tayari kupokea mafunzo ya siku nne ya namna bora za kukusanya mapato ya Serikali mkoani Morogoro leo.(Picha na Tatyana Celestine)

Katika hatua nyingine Serikali imeitaka tume hiyo ya madini nchini kuhakikisha inavuka lengo la kukusanya mapato ya  Serikali kutoka lengo lililowekwa la shilingi bilioni 310 hadi bilioni 500 ili kuhakikisha madini yanachangia pato la taifa

Amesema inashangaza kuona wakati mwingine sekta ya madini inazidiwa na sekta ya mifugo na akatolea mfano kwa kushangaa kuona Ng’ombe wanakuwa na mapato makubwa kuliko madini ambayo yana thamani kubwa.

 

Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini nchini Prof. Shukrani Elisha Manya,akiongea na Wahasibu toka sehemu mbalimbali nchini waliofika kupata mafunzo  ya namna bora za kukusanya mapato ya Serikali mkoani Morogoro leo.(Picha na Tatyana Celestine)

Naye Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini nchini Prof. Shukrani Elisha Manya, amesema Tume yake inafanya mafunzo hayo kwa wahasibu ili kuimarisha mfumo wa makusanyo na uwe wa wazi, wenye tija na kuimarisha taarifa za kibiashara za madini nchini.

Prof. Manya amesema ili kuvuka malengo ya kukusanya shilingi bilioni 500 badala ya bilioni 310 ni muhimu kwa watendaji hao wa tume kuhakikisha kunakuwa na udhibiti bora wa mapato yatokanayo na madini.

 

Mwakilishi wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof.Raphael Chibunda, Dr. Mjema akiwasilisha ujumbe aliopewa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof.Raphael Chibunda katiaka ufunguzi wa mafunzo ya namna bora za kukusanya mapato ya Serikali.

Nae Mwakilishi wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof.Raphael Chibunda, Dr. Mjema amewaasa wahasibu hao watumie fursa kufika kwa SUA kwa  kutembelea maeneo ya kihistoria yaliyopo chuoni hapo kwa siku zote wawapo katika mazingira hayo pamoja na kuwasifu kutokana na mafanikio waliyoyapata katika kukuza pato la Taifa kiuchumi hivyo ameiona kama changamoto kwa SUA kutokana na ufanisi huo kwa kuiga mfano mzuri toka kwao.

Katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko(katikati), Mwakilishi wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dr. Mjema (wa pili kushoto),Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini nchini Prof. Shukrani Elisha Manya (wa pili kulia), pamoja na wahasibu toka sehemu mbalimbali nchini baada ya ufunguzi wa mafunzo uliofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Kampasi ya Solmon Mahlangu Morogoro.

    

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner