MKOJO WA PAKA UNAVYOWANUFAISHA WAKULIMA

Na Farida Mkongwe 

Viongozi na Wakulima wa kijiji cha Mikese wamekishukuru Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kufanya utafiti uliobaini kuwa mkojo wa paka unaweza kufukuza panya wa mashambani na majumbani ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiathiri mazao ya wakulima.

Wakulima hao wakiwemo Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mikese mjini, Haji Hamisi Maridadi, Afisa Kilimo kata ya Mikese Bahati Samzugi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mikese Mohamedi Kalongwana na Mwereza Rajabu wameipongeza SUA kwa kugundua teknolojia hiyo ambayo itawaondolea matumizi ya viuatilifu walivyokuwa wakivitumia kwa ajili ya kuua panya ambao wamekuwa wakiwapa hasara kwa muda mrefu.

ice

Prof. Loth Mulungu kutoka SUA (kulia) akimuonesha mkojo wa paka uliofanyiwa utafiti Deusidedith Leornad ambaye ni Mtumishi wa Kurugenzi ya Maarifa COSTECH.(Picha na Farida Mkongwe Kulunge)

“Tumekuwa tukiingia gharama ya kununua sumu za kuulia panya ambazo wakati mwingine zimekuwa zikituathiri sisi wenyewe pamoja na kusababisha uharibifu wa mazingira lakini tangu tumeanza kutumia mkojo wa paka, panya wamekuwa wakikimbia mashambani na kuacha mahindi yakiwa salama”, amesema Bahati ambaye ni Afisa Kilimo wa kata hiyo.

Wamesema kabla ya kuanza kwa mradi huo uliogundua mkojo wa paka kuwa kinga dhidi ya panya waharibifu, panya walikuwa ni wengi sana hadi kufikia hatua ya kuwatafuna watu kwenye njayo za miguu , “tunawaomba SUA waendelee kutuletea mkojo huo wa paka ili tuweze kuutumia kwani umeonesha mafanikio makubwa kwetu”, amesema Kalongwana ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji na pia ni mkulima wa mahindi.

Kwa upande wake Profesa Mtafiti kutoka SUA Loth Mulungu amesema Mradi huo wa utafiti wa mkojo wa paka wenye lengo la kudhibiti panya waharibifu wa mazao mashambani na majumbani ulianza mwaka 2012 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi mwakani.

“Tumefanya utafiti huu ili kuwezesha mkojo wa paka kutumika kama kiuatilifu cha kufukuza panya nyumbani na kwenye mashamba na kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa”, amesema Profesa Mulungu.

Amesema zimekuwepo njia mbalimbali wanazozitumia wakulima ili kuwadhibiti panya waharibifu ikiwemo utumiaji wa sumu ambayo si rafiki wa mazingira pamoja na afya ya binadamu, “ utafiti umeonesha kuwa mkojo wa paka jike una harufu kali zaidi ukilinganisha na mkojo wa paka dume na hivyo panya wakinusa harufu tu wanakimbia wakidhani paka yupo kwenye eneo hilo na hawarudi tena”, ameongeza Prof. Mulungu.

far

Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu Dkt. Ladislaus Mnyone akiwa ofisini kwake.(Picha na Farida Mkongwe Kulunge)

Katika hatua nyingine Mtafiti huyo kutoka SUA ameishukuru Tume ya Sayansi na Teknolojia COSTECH kwa kuufadhili mradi huo na kuiomba Tume hiyo iendelee kutoa ufadhili zaidi kwa watafiti wa Tanzania ili waweze kugundua teknolojia ambazo zina manufaa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia utafiti huo Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu kilichopo SUA Dkt. Ladislausi Mnyone amesema ndani ya kituo hicho kwa sasa kuna miradi miwili mikubwa ambayo ni mradi unaolenga matumizi ya mkojo wa paka kwa ajili ya kuwadhibiti panya waharibifu pamoja na mradi wa matumizi ya mifuko maalum kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.

Dkt. Mnyone amesema kupitia miradi hiyo watafiti waliopo katika kituo hicho wameweza kupata fursa ya kufanya utafiti utakaowasaidia wakulima ambao ni miongoni mwa kipaumbele kwa taifa na hivyo kuishauri serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia kuendelea kukipatia fedha kituo hicho ili kiweze kufanya mambo makubwa zaidi kwa manufaa ya taifa.

ida

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Mikese wakifanya mahojiano na waandishi wa habari.(Picha na Farida Mkongwe Kulunge)

“Kwa watafiti wenzangu tufanye utafiti utakaowasaidia moja kwa moja watanzania, na tujitahidi utafiti tunaofanya uwafikie walengwa kwa wakati, pia katika teknolojia hizi tuhakikishe tunawashirikisha wananchi ili na wao weweze kuchangia mawazo yao, lakini tukisubiri mpaka mwisho tunaweza kuwa na teknolojia nzuri tukaipeleka kwa wananchi ikawa haiwafai, hapo tutakuwa hatujafanikiwa”, alisisitiza Dkt. Mnyome.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner