WANAFUNZI WA MWAKA WA KWANZA SUA WATAKIWA KUSOMA KWA BIDII NA KUEPUKA MAKUNDI MABAYA

   

NA: GERALD LWOMILE

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, kimewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni hapo, kuhakikisha wanafanya kilichowaleta chuoni na kuepuka makundi na kufanya mambo yanayoweza kupelekea kushindwa kufanya vizuri katika masomo au hata kufukuzwa chuoni.

Bofya hapa kwa Habari zaidi..........

 

Hayo yamesemwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma na mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Peter Gilla, wakati akizungumza na wanafunzi hao Novemba 06 2015 katika ukumbi wa “Freedom square” kampasi ya Solomon Mahlangu Manispaa ya Morogoro katika siku ya kuyajua mazingira ya chuoni.

 

Prof Gilla pia amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili kuepuka kufanya vibaya katika masomo yao na kuwataka wanafunzi hao kutumia muda wao vizuri kwa kujisoma na kuepuka kupoteza mwalekeo katika masomo.

 

Aidha amewataka wanafunzi kutumia vizuri mikopo yao na kuepuka kununua vitu vya anasa ambavyo havina faida katika masomo akitolea mfano wa kununua simu za mbwembwe badala ya kununua komputa ili ziwasaidie katika masomo.

 

“Mwanafunzi badala ya kununa komputa ambayo inaweza kumsaidia katika masomo anaenda dukani na kununua simu ya bei mbaya, radio au televisheni na mwisho anaishiwa pesa na kujikuta akishindia chipsi kavu” anasema Profesa Gilla.

 

Awali akizungumza na wanafunzi hao Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha Prof. Yonika Ngaga amesema wanafunzi ni muhimu wakajua sheria na taratibu za chuo hicho ili kuepuka kufukuzwa chuoni kwa utovu wa nidhamu.

 

“Makosa kama ya kumkarahisha mwenzako kwa matendo ya ndoa bila ridhaa yake…. Kushawishi wanafunzi wengine kugomea masomo ni baadhi ya mambo ambayo yanakatazwa katika sheria ndogondogo za chuoni na ukipatikana na hatia katika vikao halali adhabu ni kufukuzwa chuoni” anasema Profesa Ngaga.

 

Prof. Nganga ameendelea kusema kuwa ni muhimu kwa wanafunzi kujua adhabu za makosa kwa kuzisoma na kuzielewa sheria za chuoni ili kuepuka kusema wameonewa baada ya kujikuta wakipewa adhabu.

 

Zaidi ya wanafunzi elfu mbili na mia tano wanatarajiwa kujiunga na masomo katika fani mbalimbali chuo hapo.

 

 

 

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner