Mh. Samia Suluhu Hassan amewaagiza watafiti nchini kufanya tafiti na kuja na majibu

Na: Farida Mkongwe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amewaagiza watafiti
nchini kufanya tafiti na kuja na majibu yatakayosaidia kupunguza tatizo kubwa linalowakabili wakulima la
kuzalisha kwa kutumia gharama kubwa hali inayowafanya washindwe kulima kibiashara.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Agosti 8 wakati wa kilele cha maonesho ya wakulima ya nanenane
kwa Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro ambapo amewataka
watafiti kufanya utafiti utakaowapa nafuu wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija sanjari na kufikisha
matokeo ya tafiti hizo kwa wananchi.PHOTO 2019 08 07 23 53 14
“Kuna tafiti nyingi sana zinafanyika lakini nasikitika kusema kuwa tafiti hizo nyingi haziwafikii wananchi,
hivyo niwaombe watafiti kuhakikisha matokeo chanya ya tafiti zao yafike kwa wakulima ili kuwawezesha
wakulima hao kutatua changamoto zinazowakabili zikiwamo zile zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi”,
amesema Mh. Samia. 
Aidha Mh. Samia pia ameziagiza Taasisi kwa kushirikiana na Kamati mbalimbali zinazohusika na uandaaji
wa maonesho ya nanenane kote nchini kuhakikisha mabanda yote yanayohusika na kilimo, uvuvi na ufugaji
yanafanya maonesho hayo mwaka mzima ili kutoa nafasi kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji
kujifunza kupitia mashamba darasa yaliyopo katika mabanda hayo.
“Maonesho haya ni muhimu sana kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi hapa nchini, hivyo kutokana na
umuhimu wake naziagiza kanda zote nchini ikiwemo kanda hii ya mashariki kutoa huduma hii kwa mwaka
mzima na maafisa ugani nao wawepo ili elimu ya matumizi ya teknolojia za kilimo iweze kuwafikia
walengwa”, alisema Mh. Samia.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekemea vitendo vya urasimu vilivyopo kwenye wizara ya kilimo
pindi mkulima anapotaka kuuza mazao yake na kutaka  wizara iangalie upya hali hiyo kwa kuwa mkulima
naye ana haki kama walivyokuwa na haki wafanyabiashara wengine.
Katika maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki  banda la Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA
limepata zawadi ya kombe na cheti kwa kuwa mshindi wa pili wa jumla wakati zawadi ya mshindi wa
kwanza ikichukiliwa na banda la JKT na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa mshindi wa tatu.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner