VYAMA VYA WAKULIMA VIWE MSAADA KWA WAKULIMA NA SIO KUWAKANDAMIZA-BASHE

Na: Farida Mkongwe

Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe amesema wizara hiyo inapitia upya Sera ya Kilimo ili kufanya marekebisho na kuondoa kanuni na taratibu zinazomkandamiza mkulima hasa katika suala la kuuza mazao wakati wa mavuno.

picbashe

Mh. Bashe ametoa kauli hiyo wakati wa kilele cha Maonesho ya Wakulima ya Nanenane Kanda ya Mashariki ambapo amesema kuwa haiwezekani mkulima afanye shughuli zote za kilimo akiwa na familia yake lakini inapofika wakati wa mavuno na mauzo mazao hayo yanakuwa mali ya umma.

Waziri Bashe pia amesema wizara hiyo inapitia upya mfumo wa vyama vya ushirika kwa kuwa mfumo uliopo kwa sasa unamkandamiza na kumdhulumu mkulima badala ya kumtetea.

picbashe

“Ushirika sio vyama vya kidalali, kazi ya ushirika ni kuungana na kumsaidia mkulima cha ajabu na cha kusikitisha vyama vyetu vya ushirika vinaungana kumnyonya mkulima, hiyo haikubaliki hata kidogo na tayari tumeshaanza kulifanyia kazi suala hilo”, alisema Mh. Bashe.

Aidha katika kuwasaidia wakulima waweze kuuza mazao yao kwa bei nzuri Mh. Bashe amesema wizara hiyo ya kilimo imeanzaisha mfuko wa kupambana na mtikisiko wa bei za mazao pale bei hizo zitakapoanguka na ili kufanikisha hili wizara inapitia muundo uliopo na kupunguza utitiri wa taasisi zinazohitaji kodi kutoka kwa wakulima na kuzipunguza ili kuleta tija kwa wakulima.

Ameongeza kuwa maboresho mengine wanayofanya ni kuanzishwa  kwa mpango maalum wa kununua pembejeo kwa ujumla kupitia bodi zilizopo wizara ya kilimo na kuacha kununua kupitia madalali na mawakala kama njia mojawapo ya kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner