WANATAALUMA WATAKIWA KUJITOLEA KUTATUA MATATIZO YA KIJAMII

    

Na: ALFRED LUKONGE

Msemaji wa  shirika lisilo la  kiserikali la Rural Development Volunteers Associations (RDVA) linalofanya kazi za kujitolea Bw. Mathew Emilius amesema si sahihi wananchi kuiachia  Serikali peke yake kutatua matatizo ya jamii wakati kuna wimbi la wanataaluma wanaoweza kufanya shughuli hizo kwa njia ya kujitolea.

Bofya hapa kwa Habari zaidi..........

 

Bwana Emilius ameyasema hayo akiambatana na mratibu na katibu wa shirika hilo walipotembelea viunga vya SUAMEDIA mapema wiki hii  na kuongeza“shirika letu limelenga kuhamasisha jamii kujenga hali ya uzalendo kwa wanataaluma kwa kuwa ni kundi linaloaminiwa na jamii katika kuendeleza nchi”.

Amesema shirika lao limeandaa mkakati maalumu wa kuwatumia wanafunzi waliopo vyuoni na waliomaliza kutumia weledi wao kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, kuandaa makazi bora, kuimarisha miundombinu na kuandaa tafiti mbalimbali ili jamii inufaike na wanataaluma hao kwa njia ya kujitolea pamoja na kutengeneza ajira binafsi.

Kwa upande wake Bw. Julius Okanda ambaye ni katibu wa shirika hilo amesema kwa sasa taasisi yao ina wanachama kutoka SUA pekee lakini baadaye wana mpango wa kuongeza wigo zaidi ambapo pia ametoa wito kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni SUA kujiunga na RDVA ili weledi wao unufaishe jamii kwa ujumla kwa njia ya kujitolea.

Naye Bw. Emmanuel  Gasper ambaye ni mratibu wa shughuli za  shirika hilo ameongeza kwa kusema shirika lao linaamini kila mtu ana kipawa binafsi na kupitia mikakati iliyoandaliwa wanatumaini kuendeleza vipawa hivyo ili kuzalisha ajira binafsi na si kutegemea kuajiriwa.

Naye mmoja wa wanachama wa shirika hilo anayesoma mwaka wa tatu shahada ya Maendeleo Vijijini Bi. Beatrice Mushi amebainisha kuwa uananachama wake wa RDVA unamuwezesha kujiamini kwa kuwa ana uwezo wa kujiajiri mwenyewe hapo baadaye.

Mwanachama mwingine Bw. Abubakari Yusuph anayechukua shahada ya Maendeleo Vijijini mwaka wa tatu amesema  mikakati ya RDVA  ni mizuri kwenye suala la maendeleo kwa wanafunzi waliopo vyuoni kuendeleza weledi wao na kwamba wameshawahi kufanya shughuli mbalimbali mojawapo ikiwa ni kutengeneza barabara  korofi  ya Mazimbu na baadaye wakala  wa  barabara Tanzania (TANROADS) wakaanza kuikarabati kwa kiwango cha lami.

Shirika la RDVA linafanya shughuli mbalimbali za jamii ikiwemo kukarabati barabara, kusafisha hospitali na wana mpango wa kuandaa kijiji cha mfano pamoja na kufanya tafiti mbalimbali kwa njia ya kujitolea.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner