Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amekitaka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na wataalamu wake kuisaidia serikali kukifanya kilimo kiwe na mvuto

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amekitaka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na wataalamu
wake kuisaidia serikali kukifanya kilimo kiwe na mvuto ili watanzania hasa vijana waweze kuingia kwenye sekta hiyo.

Mh. Bashe ameyasema wakati wa ziara yake ya kikazi chuoni hapo kwa lengo la kuzungumza na wataalamu wa chuo
hicho na kuwakumbusha mchango wao katika kusaidia kutatua changamoto za sekta ya kilimo na kuwezesha serikali ya viwanda.
Amesema kuna haja kubwa ya taasisi zote zikiwemo Taasisi za Utafiti Tanzania (TARI), Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) na
Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu nchini (TOSCI) kushirikiana na kuwa na malengo ya pamoja ya kuhakikisha kilimo cha
Tanzania kinakuwa na faida ya kutosha.

Mhe. Bashe amesema huwezi kuzungumzia Tanzania ya Viwanda bila kuitaja SUA kwa maana ya wataalamu, utafiti na kuzalisha
wataalamu ambao ndio wanaosaidia kuwafanya wakulima waweze kuzalisha kwa tija.
Akitoa shukrani kwa Mhe. Bashe, Makamu wa Mkuu wa  Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda ameiomba serikali kuangalia
namna ya kutengeneza mazingira wezeshi balada ya kuwa na Sheria kandamizi kwenye usimamizi wa shughuli mbalimbali za
kilimo na mifugo nchini.

Akizungumzia suala la maafisa ugani amesema kuna kazi ya kubadilisha mitazamo ya maafisa ugani na wakulima ili waone
umuhimu wa kushirikiana na kutumia utaalamu walio nao maafisa ugani ili kufikia Tanzania ya viwanda.


WAKATI HUO HUO,
Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba kesho siku ya Ijumaa tarehe 11 Oktoba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye
mdahalo wa maadhimisho ya siku ya chakula duniani kwa mwaka 2019 utakaofanyika katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha
Sokoine cha kilimo SUA mkoani Morogoro
Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Raphael Chibunda amewakaribisha wadau wote wa kilimo kushiriki kwenye mdahalo huo
muhimu utakaoanza majira ya saa 3 asubuhi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya chakula dunia kwa mwaka huu ni  “MATENDO YETU, HATMA YETU. LISHE BORA KWA ULIMWENGU USIO NA NJAA”.

SUAMEDIA-BANNER

suamedia banner