Mpango kabambe wa mifugo wa Mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 ni tumaini jipya kwa wafugaji nchini

Na Calvin Gwabara

Wadau wa Sekta ya Mifugo nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango kabambe wa mifugo wa Mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 ili kuwezesha kupunguza uhaba wa nyama

na kuboresha maisha ya wafugaji nchini.
Mtaalam kutoka Dawati la Sekta binafsi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akijibu maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakati wa semina jijini Dodoma.

Wito huo umetolewa na Mtaalam kutoka Dawati la sekta binafsi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael  wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa siku mbili

ulioandaliwa na Jukwaa huru la wadau wa kilimo (ANSAF) kwa lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuripoti na kuishawishi Jamii na Serikali kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi kuboresha
sera inazosimamia.

Mtaalamu huyo amesema Tanzania imekuwa nchi ya pili kuanzisha mlango huo barani Afrika baada ya Ethiopia na hii ni baada ya kuona  Sekta ya Mifugo haijapewa kipaumbele kwenye mipango

ya nchi hususani katika sera husika.

Waandishi wa Habari za mifugo nchini wakifuatilia mada zinazowasilishwa kwenye semina ya lengo la kuwajengea uwezo wanahabari katika kuripoti na kuishawishi Jamii

pamoja na Serikali kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

 
Amesema katika mpango huo waliangalia idadi ya mifugo na Mazao yake na wakaenda mbali zaidi kuangalia  kama idadi ya kila aina ya mfugo unatoa matokeo stahiki kulingana na Mazao tarajiwa.

Mtaalamu huyo kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi ameongeza kuwa Mwaka  2016, Sekta ya mifugo na Uvuvi ilichangia asilimia 7.7 ya pato la taifa na ilikuwa kwa asilimia 2.6 huku kaya milioni 4.6

zilionekana kujishughulisha na mifugo.

Aidha ameongeza kuwa  Nyama nyekundu na nyeupe zinachangia kwa asilimia 40% kwenye pato la taifa, Maziwa asilimia 30% huku aina nyingine za Mazao ya mifugo zikichangia asilimia 30.


Amesema kuwa matokeo ya utafiti huo walioufanya wamegundua kuwa mahitaji ya nyama ni makubwa kuliko uzalishaji, vilevile kwenye maziwa lakini changamoto kubwa ni Magonjwa,
malisho, maji pamoja na Mbari (Breed).
 
Washiriki na Viongozi wa ANSAF wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mwenye miwani mstari wa mbele) Bw.Amos Zephania 
Bwana Michael amesema kufikia mwaka 2032 upungufu wa nyama nyekundu utakuwa tani 1,731,000 Sawa na asilimia 33 ya mahitaji huku eneo lililotengwa kwenye ufugaji ni asilimia 9.4 ya eneo la Taifa.

Ametoa wito kwa waandishi wa habari kujikita katika kutangaza Sekta ya Uvuvi na Mifugo pamoja  fursa zilizopo ili jamii iongeze kasi ya kushiriki na kutumia mazao yake yanayozalishwa kikamilifu

 kutoka kwenye sekta hiyo .

Sekta ya Mifugo inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 7.9 ya pato la taifa

Na Calvin Gwabara

Dodoma

Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bwana Amos Kulwa Zephania amesema Sekta ya mifugo inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 7.9 ya pato la taifa   ya sasa endapo Serikali na wadau wengine watawekeza zaidi katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo

Amos Kulwa Zephania ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi  wa habari za mifugo nchini kutoka vyombo mbalimbali vya habari iliyoandaliwa na Shirika la ANSAF ili kujadili changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta hiyo hapa nchini.

Bwana Zephania amesema pamoja na Tanzania kuwa nchi ya pili kwa wingi wa mifugo barani Afrika baada ya kugawanywa kwa nchi ya Sudan lakini bado mifugo inachangia asilimia ndogo kwenye pato la taifa huku ikikua kwa asilimia 4.9 tu.

Mgeni Rasmi ANSAF

Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi bwana Amos Kulwa Zephania (Katikati) Akitoa neno kwa wanahabari(hawapo pichani) wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa waandishi nguli wa habari za mifugo nchini kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

“Kwa makadirio yetu mwaka 2020 tutakuwa na Ng’ombe milioni 32.2, Mbuzi milioni 20, Kuku wa asili na wa kisasa watakuwa milioni 79.1 na nguruwe milioni 2 hivyo lazima tujiulize rasilimali  hizi zote zinatusaidia nini na kama uzalishaji wetu wa maziwa kwa mwaka ni lita bilioni 2.7 wakati matumizi yetu ni asilimia 47 kwa mwaka” Alisema Zephania.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa watu hawatumii bidhaa za ndani zinazotoka kwenye mifugo hivyo waandishi wa habari wasaidie kutoa elimu juu ya faida zinazotokana na bidhaa zetu za ndani huku akibainisha kuwa Wizara inafanya mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo ili kuhakikisha inatoa mchango unaostahili katika pato la taifa lakini kwa wafugaji na washiriki wa nyororo  wa thamani wa mifugo.

Amesema kupitia oparesheni Zagambo ya kukamata bidhaa feki za mifugo kutoka nje na zilizoisha muda wake ambazo zinaathari kubwa kwa afya ya binadamu kumewezesha kupata zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa mwezi kupitia aparesheni hiyo nchini.

Amesema hivi sasa serikali imekamilisha na kuanza kurekebisha mpango kabambe wa mifugo Tanzania ambao umelenga kuhakikisha afya ya mifugo kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa na chanjo za mifugo kwa urahisi ili kufikia soko la kimataifa hasa baada ya kuona mazao mengine ya mifugo hayaruhusiwi kuingia kwenye masoko ya nchi mbalimbali duniani.

Mkurugenzi ANSAF

Mkurugenzi Mkuu wa ANSAF bwana Audax Rukonge akitoa neno kwa wanahabari (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.

Pia amesema mpango huo umezingatia swala la kuboresha malisho kwa wafugaji ili kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuhakikisha swala la uhamilishaji wa mifugo linapewa nafasi ili kupata aina za mifugo inayohitajika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ANSAF Bwana Audax Rukonge akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo amesema fursa zinaendelea kutokea kila siku lakini watu hawaziangalii na kuzichangamkia.

“Hivi karibuni tunatarajia Afrika kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia na idadi kubwa ya watu watakaokuja watahitaji Nyama, Mayai na Maziwa hivyo lazima tujipange ili wakati huo ukifika na sisi tukauze bidhaa zetu baada ya kukosa fursa kama hiyo mashindano hayo yalipofanyika Afrika ya Kisini” Alisema Rukonge.
Waandishi ANSAF 2

Wanahabari wakifuatilia neno la ufunguzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Mifugo na uvuvi.

Mkurugenzi huyo wa ANSAF amesema sekta hiyo inahitaji uwekezaji wa serikali, sekta binafsi na wadau wengine ili iweze kutoa tija inayotakiwa huku akibainisha maeneo ya fursa kuwa ni katika unenepeshaji wa mifugo,Madawa ya mifugo na Chanjo,Uhamilishaji (breeding) pamoja na uzalishaji wa chakula cha mifugo.

Akizungumzia lengo la warsha hiyo ya siku mbili kwa wanahabari hao Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ANSAF Bw. Mbarwa Kivuyo amesema ni kutaka kukumbushana na kuelimishana juu ya changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta ya mifugo na kuona namna ya kuzitumia fursa hizo katika kuleta matokeo makubwa.

Wanafunzi wa SUA mbioni kupata ufumbuzi wa tatizo la viwavijeshi

Na, CALVIN  E. GWABARA
Wanafunzi wa wanne  wa Mwaka wa tatu kutoka chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wanaofanya tafiti shirikishi kwa kushirikiana na wakulima katika kupata ufumbuzi wa matatizo
ya wakulima wa Mahindi Mkoani Morogoro kwa kutumia mbinu za asili kwa ufadhili wa Shirika la Kilimo Endelevu SAT wako mbioni kupata ufumbuzi wa tatizo la Viwavi jeshi vamizi.
 

Mwanafunzi Gloria Francis ( Mwenye Koti la Blue) akifafanua jambo kwa wakulima kuhusu utafiti wake wa kina cha shimo linalofaa kupanda mahindi.
 
Wakiongea na Waandishi wa habari katika eneo wanalofanyia utafiti kwenye shamba la SUA mmoja wa wanafunzi hao Matha Makumba anayefanya utafiti wa kutumia
Unga wa majani ya  Mlonge,Unga wa mbegu za Muarobaini na mchanganyiko wa mlonge na Muarobaini amesema kuwa matokeo ya awali yanaonesha Muarobaini umefanya vizuri.
 
Mwanafunzi huyo mtafiti amesema pamoja na kwamba muarobaini umefanya vizuri lakini bado kuna mashambulizi ya wadudu hao pamoja na kupuliza dawa hiyo kila baada ya wiki
moja hivyo utafiti zaidi unatakiwa kufanyika kuweza kujua ni kwa namna gani maji ya mmea huo yanaweza kuboreshwa ili kupambana na wadudu hao.

Newton Kilasi Mhadhiri SUA na msimamizi wa wanafunzi hao (Kulia) akifafanua jambo.
Pamoja na swala la matumizi ya mbinu hizo za asili lakini pia walipanda mbegu tofauti tatu kuweza kubaini ni mbegu gani inayoweza kustahimili au kutoshambuliwa na
wadudu hao ambapo walipanda mbegu aina za Staha,Meru na Tumbili lakini mbegu ya Tumbili imeonekana kutoshambuliwa zaidi na wadudu hao ikilinganishwa na mbegu
hizo nyingine.
 
Kwa upande wake Glory Francis mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika ndaki ya Kilimo  SUA ambaye amefanya utafiti kuona kina gani cha shimo kinatakiwa kupandwa mbegu
ya mahindi ili iweze kuota vizuri baada ya wakulima kulalamika kuwa mbegu wanazopanda hazioti huku kukiwa na utofauti wa uchimbaji wa mashimo amesema kuwa yeye amebaini
kuwa shimo la urefu wa sentimita tano ndilo linalofaa kupandwa mbegu.
Bi. Matha Makumba Mwanafunzi Mtafiti kutoka SUA anayefanya utafiti wa mbinu za asili za kukabiliana na Viwavijeshivamizi.
Aidha amesema yeye alipanda kwenye mashimo ya urefu wa setimeta 15. 5 na sentimita 3 ili kuweza kujibu changamoto hiyo ya wakulima kutokana na wakulima hao kuwa na
uchimbaji tofauti wa mashimo wengine yakiwa marefu na mengine mafupi lakini katika utafiti huo amebaini kuwa mbegu kubwa zimefanya vizuri kwenye sentimita 5.
 
Hata hivyo ameshauri wakulima kutumia mbegu kubwa kama ni msimu mzuri wa mvua kwani zinaweza kuota vizuri na kukua huku akishauri wakulima kuachana na kurudia mbegu
za msimu uliopita na badala yake kila mwaka waende dukani kununua mbegu kwani kurudia mbegu kunapoteza sifa za mmea na kushusha uzalishaji.

 

Wakulima kutoka vikundi mbalimbali wakipata  maelezo kutoka kwa mwanafunzi mtafiti wa SUA
 
Kwa upande wake mtafiti Neema Erasto  ambaye anafanya utafiti wa kujua kwanini kunakuwa na uotaji hafifu wa mbegu amesema walitumia mbegu za asili na mbegu za dukani
lakini pia kwa kutumia mbinu mbadala kwa kuloweka mbegu kwenye chumvi na kuloweka kwenye maji yasiyo na chumvi.
 
Amesema utafiti wake umebaini kuwa mbegu zilizolowekwa kwenye maji yasiyo na chumvi zimeota vizuri kuliko zile ambazo zililowekwa kwenye maji ya chumvi na zile ambazo
hazikulowekwa kwakuwa zilizibeba unyevunyevu wa kutosha na zilipofika ardhini zimeota kirahisi zaidi na haraka.
 
Amesema zile zilizolowekwa kwenye chumvi zimeota kidogo kwakuwa zinapofika ardhini kunakuwa na ukizani wa kuvuta maji na hivyo kusababisha mbegu kuchelewa kuota na
hivyo kuwashauri wakulima kutoloweka mbegu kwenye maji ya chumvi kama wanavyofanya na waloweke kwenye maji siku moja kabla ya kuzipanda ili zileinike na kuota haraka.
 
Akizungumzia utafiti huo wa wanafunzi hao Mtaalamu kutoka shirika la Kilimo endelevu SAT Bi. Elizabeth Girangai amesema shirika lao lina utaratibu wa kufanya tafiti shirikishi
kwa kushirkiana na watafiti wa SUA kwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoletwa na wakulima.
 
Amesema awamu ya kwanza waliwakutanisha wakulima na wafunzi na kisha wakulima wakaeleza changamoto zao ambapo wanafunzi hao wa SUA walipata maeneo ya kufanyia utafiti
na kisha SAT kuwawezesha kutafuta ufumbuzi kwa kushirikiana nao kuanzisha mwanzo hadi mwisho na sasa wanawaleta wakulima kuona maendeleo.
 
Baada ya matokeo hayo kukamilika mwaka huu wataitisha mkutano mkubwa kwa kuwakutanisha pamoja wakulima,maafisa ugani na viongozi wa vijiji ili waweze kusikia na kujadiliana
kwa pamoja namna nzuri za kutumia matokeo hayo yatakayotolewa na wanafunzi hao ili kuboresha kilimo chao.
 
Akizungumzia utafiti huo mmoja wa wakulima washirki wa utafiti bwana Manase Thomas kutoka kijiji cha kimambira ambaye ni mkulima wa kilimo hai amesema wamefurahia utafiti
huo kwani unakwenda kujibu changamoto walizoziwasilisha kwa SAT na hivyo kutasaidia kuboresha kilimo chao.

Amesema mbuni zote zilizotumiwa na watafiti hao zimeleta matokeo chanya hasa katika matumizi ya mbuzu za muarobaini katika kuua viwavijeshi vamizi huku akiwataka wakulima
wenzake wanaopenda kutumia mbegu walizovuna msimu uliopita sasa kuchagua mbegu nene na sio zile ndogondogo maana zinakuwa dhaifu.

Subcategories

Page 9 of 52