MAYANGA WA MBAO FC ATUMIA DAKIKA 270 KUPATA POINT TATU TPL

 
KOCHA Mkuu wa Mbao FC, Salum Mayanga na msaidizi wake, Novatus Fulgence wametumia dakika 270 kupata pointi tatu, baada ya kukabidhiwa timu mwezi Marchi mwaka huu wakichukua mikoba ya Ally Bushir.
Mayanga alianza kazi kwa kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba mchezo uliochezwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro, akapoteza mbele ya Biashara United Uwanja wa  CCM kirumba kwa kufungwa bao 1-0 kabla ya kutoka suluhu na Azam FC ya Dar uwanja wa CCM kirumba.
Juzi alivuna pointi tatu mbele ya Ndanda uwanja wa CCM Kirumba baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Said Junior ambaye kwa sasa amefunga jumla ya mabao nane kwenye ligi.
Hivyo Mayanga ametumia dakika 270 kuvuna pointi tatu ambazo zimemuondoa kutoka nafasi ya 19 aliyokuwa akishika mpaka kufika nafasi ya  13 kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 34 wamejikusanyia pointi 40. 

Hizi Ndizo Sehemu utakazopita mwili wa Dr. Mengi LeoRatiba ya kuupokea mwili wa Dr. Reginald Mengi, Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere imeelezwa kuwa itafanyika kesho, Jumatatu, saa 8:00 mchana.

Mwili wake utaletwa na ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kutokea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).

Baada ya mwili kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa JNIA, utapitishwa maeneo ya Tazara, Buguruni, Ilala, Kigogo, Magomeni hadi Kinondoni.

Kutoka Kinondoni, mwili wake pia utapitishwa hadi katika maeneo ya Morocco, barabara ya Bagamoyo, Sayansi, Mwenge hadi katika hospitali ya Lugalo ambako mwili wa Dr. Reginald Mengi utahifadhiwa.

Ratiba hiyo itaendelea siku ya Jumanne ya Mei 7, 2019, ambapo mwili utapelekwa katika ukumbi wa Karimjee, kwaajili ya watu wote kuuaga na kisha utarejeshwa nyumbani kwake. Siku ya Jumatano mwili utasafirishwa kupelekwa Moshi Machame ambako Ibada ya mazishi itafanyika siku ya Alhamis katika kanisa la Kisereni (KKKT).

Watahiniwa 91,442 Wa Kidato Cha Sita Kuanza Mitihani Ya Taifa Leo

Watahiniwa 91,442 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita kuanzia kesho Jumatatu Mei 6 hadi 23, 2019.
Mbali na hao, watahiniwa 12,540 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kozi ya ualimu katika ngazi ya cheti na stashahada.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Mei 5, 2019 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde, amesema kumekuwa na ongezeko la watahiniwa wa shule wanaomaliza mtihani wa kidato cha sita kwa asilimia 4 ikilinganishwa na mwaka jana huku idadi ya watahiniwa wa ngazi ya ualimu wakiongezeka kwa asilimia 41.
Akitoa ufafanuzi wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha sita waliosajiliwa mwaka huu, amesema kati 80,305 ni watahiniwa wa shule na 11,117 ni wa kujitegemea
“Katika watahiniwa wa shule kati yao 46,224 sawa na asilimia 57.56 ni wavulana na 34,081 sawa na asilimia 42.44 ni wasichana huku watahiniwa walio na uhitaji maalumu wapo 102 kati yao, 67 ni wenye uoni hafifu; 16 ni wasioona; 18 wenye ulemavu wa kusikia; na 1 ni mwenye ulemavu wa afya ya akili,” amesema Dk Msonde.

WAAJIRI WATAKIWA KUTENDA HAKI KWENYE MALIPO YA WAFANYAKAZI WAO

Rai imetolewa kwa waajiri mkoani Morogoro kuwalipa wafanyakazi wao mishahara kulingana na thamani halisi ya mapato yanayozalishwa bila kujali kima cha chini kilichowekwa na Serikali.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Kebwe Stephen Kebwe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani ,Mei Mosi yaliyo fanyika kimkoa ndani ya manispaa hiyo katika uwanja wa Jamhuri na kuongeza kuwa mahali pa kazi panapaswa kuwa sehemu yenye upendo na mahusiano mema baina ya mwajiri na mwajiriwa ili kutoa tija inayokusudiwa.
Aidha Mh. Kebwe amewashauri wafanyakazi kujiandaa kustaafu vizuri wakiwa bado katika utumishi  kwa kuangalia na kutumia fursa hasa upande wa kilimo kwa kuwa mkoa huo wa morogoro una ardhi nzuri na yakutosha sanjari na hali ya hewa inayofaa kwa kilmo.Akisoma risala katibu wa chama cha wafanyakazi  wa sekta ya mawasiliano ya simu Bw. Cloud Kobero ameainisha changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ubinafsishaji wa ndani kwa ndani wa viwanda na kushindwa kuwalipa wafanyakazi vizuri na kwa wakati, waajiri kutoa mikataba mifupi mifupi kwa wafanyakazi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.


Katika  hatua nyingine Naibu wa  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taaluma Prof. Peter Gillah aliyemuwakilisha Makamu wa Mkuu  wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amewahakikishia wafanyakazi wa taasisi hiyo kuwa menejimenti inatambua changamoto zao na kuahidi kuwa inaongeza kasi katika utatuzi wa changamoto hizo.

Amesema wafanyakazi ni wajibu kufanya kazi kwa bidii na kuepuka majungu  kabla ya kudai haki huku akiwapongeza wafanyakazi bora 52 na wafanyakazi hodari 6 ambao wameonekana kufanya vizuri katika utendaji wao wa kazi.


Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani MEI MOSI kitaifa yamefanyika mkoani Mbeya huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli yakiwa na kauli mbiu isemayo “tanzania ya uchumi wa kati inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa.

LIVE: JPM Akiendelea na ziara yake MBEYA

JPM Awaka! Mliokula Hela mtazitapika....

Rais Magufuli Atuma Salamu za Pole Kufuatia Kifo cha Mzee Reginald Mengi

Rais Magufuli ametuma salamu za Pole kwa familia na Wafanyakazi wa IPP Media kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo.
 
 Mengi amefariki dunia usiku wa kuamkia Leo Mei 2, 2019 akiwa Dubai
 
"Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na Rafiki yangu Dkt. Reginald Mengi. Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa ktk maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo ktk kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabishara. "Ameandika Rais Magufuli

BREAKING: Mwenyekiti wa makampuni ya IPP Dr. Reginald Mengi amefaiki dunia

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP , Dkt Reginald Abraham Mengi (75) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.

Dk Mengi amefariki dunia akiwa jijini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Dk Mengi alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa barani Afrika, ambapo sehemu ya utajir wake aliuelekeza kwa jamii kwa kutoa misaada mbalimbali.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes mwaka 2014, utajiri wa bilione huyo ulitajwa kuwa ni TZS trilioni 1.3 ($560 milioni).

Enzi za uwahi wake na katika shughuli zake aliweza kushinda tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa, pamoa na kuandika kitabu chake cha I Can, I Must, I will.
 

Mungu Ailaze Roho yake Mahali Pema Peponi. Amina

Rais Magufuli awataka wafanyakazi kuwa wavumilivu kuhusu nyongeza ya mishahara

Rais Magufuli amesema kuwa hatoongeza mshahara mwaka huu, kwani ahadi yake ya kupandisha mishahara katika uongozi wake haijaisha kwa sababu bado hajamaliza muda wake madarakani.
 
 
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo May 1, 2019 mara baada ya hapo awali TUCTA kumuomba atimize  ahadi yake ya kuwaongeza wafanyakazi mishahara.

Niwaambie ndugu zangu, Katibu mkuu TUCTA alinikumbusha kuhusu ahadi yangu, ninaikumbuka na ninasema muda wangu bado nipo madarakani, ninachoomba muwe na subira.

Ni kweli kwenye sherehe kama hizi mwaka jana niliahidi kuwa nitaongeza mishahara ya wafanyakazi kabla sijaondoka madarakani, ndugu zangu tuvumilie tu sikutaka kuwadanganya hapa kuwa nimewaongezea mishahara halafu fedha mtakazozipata hazipo, nyinyi endeleeni kuvumilia tupo katika muelekeo mzuri wa suala hili”, Amesema Rais Magufuli na kuongeza;


“Ningeweza kuwaongezea elfu 5 au 10, kesho tu bidhaa zingeanza kupanda hivyo lazima kwanza tujenge uchumi imara. Mimi mwenyewe nilikuwa mwalimu na nikaenda kuoa mwalimu anayejua shida zetu Serikali inawapenda wafanyakazi.

Waziri Mhagama Awaonya Waajiri Wote Kutonyanyasa Wanawake

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista mhagama amewataka waajiri wote nchini kutonyanyasa wanawake katika masuala ya kazi ili kuwa na usawa maeneo ya kazi.

Ameitoa kauli hiyo hii jana tarehe 30 Aprili, 2019 alipokuwa akifungua semina ya siku moja ya viongozi wanawake kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini walipokutana kujadili masuala yanayowahusu wawapo kazini ikiwemo; haki na wajibu wao wawapo kazini iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Paradise Inn Jijini Mbeya.


Waziri alieleza kuwa waajiri hawana budi kubadili mitazamo hasi iliyopo katika jamii ya kuona wanawake ni viumbe dhaifu na wenye majukumu mengi yanayoweza kukwamishi jitihada zao wawapo kazini badala yake wawaone kuwa ni viungo muhimu katika kuchangia uzalishaji na maendeleo nchini.

“Mchango wa wanawake ni mkubwa endapo utatambuliwa na kuthamini katika nyanja zote za ukuaji wa uchumi, hivyo ni vyema maeneo ya kazi waajiri watimize wajibu wao kwa kundi hili kwa kuzinigatia sheria zilizopo na wasinyanyaswe na waendelee kuheshimiwa na kupewa haki na stahiki zao kama wafanyakazi wengine.”alisisitiza Waziri Mhagama.

Waziri alieleza jitihada za serikali ni kuhakikisha inasimamia vyema sheria na taratibu za kazi nchini kwa kuliangalia kundi hili ili kuwa na waajiriwa wenye kuzingatia usawa wa kijinsia.


“Ninakemea vitendo vya unyanyasaji wa haki za wanawake kazini ikiwemo kukoseshwa haki zao na vyama hivi vya wafanyakazi viendelee kuleta tija katika kukemea matendo hayo,”alisistiza Waziri Mhagama.

Aidha Waziri aliwataka wanawake kuendelea kuvitumia vyama vya wafanyakazi kama jukwaa maalum la kueleza na kutatua changamoto zao.

Aliongezea kuwa, pamoja na changamoto wanazokutana nazo wanawake hawana budi kujiendeleza kielimu ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo katika masuala ya kazi.

“Wanawake umefika wakati kuendelea kujiendeleza katika eneo la elimu ili kuwa na vigezo mahususi vitakavyo wapa nafasi nzuri katika maeneo yenu ya kazi.”alisisema Waziri Mhagma.

Naye rais wa Shirikizo la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya alimpongeza waziri pamoja na changamoto zilizopo katika kufikia haki sawa kwa wote , alieelza umuhimu wa kuendelea kuliinua kundi hili ili kuwasaidia wanawake wa Kitanzania katika kupata haki na usawa kwenye maeneo yao ya kazi.

“Wanawake wana uwezo mkubwa hivyo tuendelee kujali na kutunza nafasi zao wawapo kazini ili kuwezesha Taifa kuendelea kuwa na maendeleleo,” alisisitiza Nyamhokya.

Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Wanawake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Bi. Rehema Ludanga alieleza kuwa, ni wakati sahihi kuendelea kuchangamkia fursa za maendeleo ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya wanawake vitakavyosaidia kuondokana na hali ya utegemezi na kuchangia katika ongezeko la uzalishaji nchini.

Subcategories

Page 4 of 44