Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) yafanikisha mkutano wa Bodi Mpya

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya kujiendeleza (ICE), Prof. Caroline Nombo (wa pili kushoto) amewaomba wajumbe wa bodi ya ICE kuhakikisha wanaisaidia Taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa kuitangaza SUA na kazi zake kwa jamii na wadau mbalimbali.

 

Ombi hilo amelitoa wakati akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya ICE itakayodumu kwa kipindi cha mwaka 2017-2019. Bodi ya ICE inajumuisha wajumbe kutoka ndani na nje ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Wajumbe kutoka nje ya chuo ni pamoja na Bwana Francis Sabuni, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains Conservation Endowment Fund (EAMCEF). Mjumbe mwingine kutoka nje ya SUA ni Dkt. Ernest Mwasalwiba kutoka chuo kikuu Mzumbe. Wajumbe wa Bodi kutoka ndani ya Chuo ni Prof. Nombo (Mwenyekiti), Dk. Fatihiya Masawe, Dk. Innocent Busindeli, Ndg. Kassim Ramadhani na Prof. Loth Mulungu.

 

Prof. Nombo amesema anaamini Bodi hiyo itasaidia kutoa maelekezo, miongozo, mapendekezo na ushauri wa namna ya kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya ICE unafanikiwa.

Kumekuwepo na maswali mengi kutoka kwa watunga sera,wakulima,wanasiasa na wadau wa kilimo nchini kutaka kuelewa zaidi nafsi ya SUA katika kufanya tafiti, kuzalisha bunifu na teknolojia,  mafunzo na huduma mbalimbali zinazotolewa na Chuo.   Kuna maswali mengi ambayo SUA inatakiwa kutoa majibu yake ikiwemo kwanini wakulima wengi katika nchi yetu bado wanatumia mbinu duni katika kilimo na ufugaji. Ni jukumu la bodi kuishauri SUA kupitia ICE ili Chuo kipate majibu ya changamoto za kuendeleza kilimo nchini”,  Alisisitiza Prof. Nombo.

“Tuliona ni vema tuwe na wajumbe wa aina yenu kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya kitaalam ili kushirikiana katika kubadirishana uzoefu ili kufikia kazi za Chuo zitatambulike zaidi kwa umma.’’ Aliongeza Prof. Nombo.

Akitoa taarifa za mpango wa kuboresha masafa ya SUATV na SUAFM, Mkuu wa kitendo cha vyombo vya habari za SUA (SUAMEDIA) Ndg. Libuhi Salehe aliiambia bodi kuwa Uongozi wa Chuo unaendelea na mchakato wa kuiwezesha SUATV kurusha matangazo yake moja kwa moja kutoka Morogorokupitia ving’amuzi mbalimbali. Kwa sasa, SUATV inapatikana katika king’amuzi cha TING, Channel 50. Ilielezwa pia kuwa Chuo kipo katika maandalizi ya mwisho ya kuongeza masafa ya SUAFM (101.1) ili radio izidi kusikika vizuri zaidi na kuwafikia wasikilizaji wengi.