Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE), kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), imeendesha mafunzo ya siku nne (4), juu ya ufugaji bora wa kuku, yakiwakutanisha wafugaji wa kuku na wajasiriamali kutoka mikoa ya Morogoro, Dodoma,Pwani(Kibaha).Dar es Salaam. Moshi na Tabora. Mafunzo haya yalilenga kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu mbinu bora na za kisasa za ufugaji wa kuku, kwa lengo la kuongeza tija na ubora wa katika sekta ya ufugaji wa kuku. Washiriki pia walitoka katika taasisi mbalimbali zikiwemo Wipaz Kibaha na Farmer Pride Tanzania, wakinufaika na elimu ya nadharia pamoja na vitendo. Katika sehemu ya vitendo, walipata fursa ya kutembelea kiwanda cha chakula cha kuku cha TANFEED LTD, kilichopo eneo la Modeco hapa manispaa ya Morogoro, ambapo walijifunza juu ya uzalishaji wa chakula bora cha kuku,kuona na kujifunza aina mbalimbali za cages za kufugia kuku na namna bora ya kuchanganya aina tofauti za vyakula ili kupata aina moja ya chakula kwa makundi tofauti ya kuku pia kutembelea shamba la Bi. Fatuma Mtandu anaeishi eneo la Mkambarani, nje kidogo ya manispaa ya Morogoro, ambapo walijionea namna bora ya ufugaji wa kuku na kwa utaalamu unavyoweza kuleta mafanikio makubwa. Kupitia mafunzo haya, SUA inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya dhati ya kuhamasisha kilimo na ufugaji wa kisasa, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuinua uchumi wa mfugaji mdogo na mjasiriamali wa ndani katika kuchangia maendeleo ya Dira ya Taifa .2025-2050.

