Matokeo ya Mafunzo ya Muda Mfupi ya Ufugaji wa Kuku Yanayotolewa na SUA

1. Utangulizi

Ufikiaji wa matokeo tarajiwa ya mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa kuku yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) ni jambo muhimu linalopendwa na SUA pamoja na washiriki wa mafunzo wanaotoka katika jamii yetu. Makala hii (ambayo pia ipo katika lugha ya Kiingereza ukibonyeza bendera ya Tanzania kwenye ukurasa wa mbele wa tovuti ya ICE) inaangazia ushuhuda wa mwandishi wa makala hii na mrejesho unaoletwa na washiriki wa mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa kuku yaliyotolewa hivi karibuni na ICE kwa kushirikiana na Idara ya Sayansi za Wanyama, Viumbehai Majini na Nyanda za Malisho (DAARS), Ndaki ya Kilimo (CoA).

Washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kuku kibiashara wakionesha vyeti vyao vya ushiriki baada ya kumaliza mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na SUA kwa ufadhili wa Shirkila la Chakula Duniani (FAO) katikati ya Mwezi Januari 2021, Bihawana Mkoani Dodoma

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji kuku waliojigharamia wenyewe gharama za mafunzo wakipiga picha na wawezeshaji wa mafunzo yaliyofanyika ICE, SUA mwishoni mwa mwaka 2020

2. Mafunzo Yaliyotolewa

Kati ya mwezi Octoba 2020 na mwezi Februari 2021, SUA kupitia ICE kwa kushirikiana na Idara ya Sayansi za Wanyama, Viumbehai Majini na Nyanda za Malisho (DAARS), CoA ilifanya mafunzo ya muda mfupi ya siku nne hadi tano kuhusu ufugaji wa kuku yaliyohudhuriwa na washiriki karibia 90, kati yao wanawake  wakiwa asilimia 40%. Kozi tatu za ufugaji wa kuku zilizofadhiliwa na FAO zilijumuisha mafunzo ya ujasiriamali ambayo yalitolewa kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Uchumi Kilimo na Stadi za Biashara (SAEBS) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Lengo kuu la mafunzo hayo ilikuwa ni kuwapatia elimu na ujuzi wakulima na wajasirimali ili waweze kuboresha na kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku na hivyo kuweza kujiajiri

Mada zilizofundishwa ni kama ifuatavyo:

 • Mifumo ya ufugaji
 • Ujenzi wa mabanda
 • Namna ya kuanzisha mradi
 • Utotoleshaji na utunzaji vifaranga
 • Lishe na vyakula
 • Ufugaji kuku wa kienyeji na chotara
 • Ufugaji kuku wa nyama
 • Ufugaji kuku wa mayai
 • Magonjwa ya kuku na vyanzo vyake
 • Udhibiti wa magonjwa (bio-security)
 • Uwekaji kumbukumbu
 • Soko na biashara
 • Ufugaji huria
 • Ufugaji huria ulioboreshwa
 • Ufugaji mdogo mabandani
 • Ufugaji wa kati na mkubwa

Mwezeshaji, Prof. Said Mbaga (aliyesimama mbele ya darasa) akijadiliana na washiriki wa mafunzo ya ufugaji kuku wakati wa kipindi kimojawapo huko Bihawana, Dodoma

Kuku wa mayai wanaofugwa na Ten Youth Group Enterprises (Kwa Kiswahili: Mradi wa Vijana Kumi) kama walivyoshuhudiwa wakati wa ziara ya mafunzo ya washiriki jijini Dodoma

 

3. Katika Picha: Matokeo ya Mafunzo ya Muda Mfupi ya Ufugaji wa Kuku Yanayotolewa na SUA

Jitihada za mkulima katika manispaa ya Morogoro zikionesha vifaranga 200 vya kuku wa kienyeji alivyofuga baada ya kuhudhuria mafunzo ya ufugaji wa kuku ICE, SUA

  

Utunzaji wa vifaranga 450 vya kuku wa mayai unaofanywa na Best Women Group-Mlebe (Kwa Kiswahili: Kikundi Bora cha Wanawake-Mlebe) katika kijiji cha Mlebe wilaya ya Chamwino baada ya wanachama wao wawili kuhudhiria mafunzo ya SUA ya ufugaji wa kuku yaliyofantika katika jiji la Dodoma

Mashine ya kutotolesha iliyotumiwa na mshiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kuku anayefuga kuku wa kienyeji 1000 Rufiji. Mshiriki huyu alinunua vifaranga 700 aina ya Kuchi kutoka mkoani Mtwara kwa bei ya shilingi 1500 kwa kila kifaranga huku vifaranga wengine akiwapata kwa kutotolesha kwa mashine.

 

Kwa maelezo zaidi kuhusu makala hii tafadhali mwandikie Dk. Innocent H. Babili: ibabili@sua.ac.tz