Maonesho ya Teknolojia, Bunifu, Tafiti na Mkutano wa Kisayansi Yatia fora katika Wiki ya Kumbukizi ya Sokoine, SUA, Morogoro, Tanzania

Kutoka kwenye sakafu ya moyo, pongezi nyingi ziwaendee Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Wanasayansi na Wadau wote wa SUA kwa mafanikio yaliyopatikana katika maonesho ya kuvutia sana ya teknolojia, bunifu na kongamano la kisayansi wakati wa wiki ya Kumbukizi ya Sokoine hapa chuoni kwetu.

Pongezi nyingi kwa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhamilishaji wa Teknolojia, na Ushauri wa Kitaalam (DPRTC) kwa kuendesha vema kongamano la kisayansi ambalo lilipokea maandiko yenye kuongeza maarifa yaliyowasilishwa katika Kongamano la Pili la Kisayansi, SUA lililofanyika tarehe 25-26 Mei 2021.

Picha: Prof. Esron Karimuribo, Mkurugenzi wa DPRTC SUA, akiongea jambo wakati wa Kongamano la Pili la Kisayansi, SUA lilifanyika ICE, SUA (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya).

Kongamano hili lilisisimua hisia chanya za kisayansi na hekaheka za kupishana washiriki mara huku mara kule wakati wa kwenda kwenye vyumba tofauti ambako mada mbalimbali ziliwasilishwa kulileta radha ya aina yake ya kufurahisha sana.

Picha:  Bango la Kongamano la Pili la Kisayansi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo uliofanyika tarehe 25-26 Mei 2021 (Picha, shukrani kwa Lucy Madala)

Picha: Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia, na Bunifu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula (Katikati) na sehemu ya Uongozi wa SUA  (waliokaa mstari wa mbele), wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano la Pili la Kisayansi la SUA lililofanyika tarehe 25 – 26 Mei 2021 katika Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE), SUA, Morogoro, Tanzania (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya)

Ilikuwa ni wiki ya SUA kwa kweli. Ni wiki inayoacha kumbukumbu nzuri na ya kupendeza kichwani.  Ilikuwa fursa adhimu ya kuonesha na kuendelea kuthibitisha umahiri wa SUA katika safari ya kuongoza maendeleo ya sayansi nchini na nje ya mipaka yetu.

Tumefahamu mengi na mapya mazuri sana katika wiki hii. Kwa kutaja machache, Dr. Florence Turuka kati ya mengi alitumegea njia bora ya kukokotoa GDP, Prof. Gerard Misinzo alitushirikisha namna ya kukishinda kirusi kinachosababisha ugonjwa wa Korona. Halafu ilikuwa ni ala! kumbe mafuriko ya mito, siyo mvua ya mahala husika, yanafaida katika sehemu zenye ukame katika kuongeza kiasi cha maji chini ya ardhi- muhimu katika kupatikana maji ya visima. Haya yaliwasilishwa kidijitali na Prof. Richard Taylor wa Ndaki ya Chuo Kikuu cha London, aliyeshirikiana na Prof. Japhet  Kashaigili wa SUA katika kazi yake.

Picha: Dk. Florence Turuka (aliyeshika kipazasauti), akiwasiliana kwa makini na hadhira wakati wa wasilisho lake ambalo lilikuwa moja ya mada kuu katika Kongamano la Pili la Kisayansi, SUA lililofanyika ICE, SUA. Aliyekaa karibu na kushoto kwa Dk. Turuka ni Prof. Sebastian Chenyambuga wa SUA- ambaye katika Kongamano hilo aliwasilisha mojawapo ya mada kuu kuhusu “Bunifu zinazochangangia katika Uzalishaji Endelevu wa Mifugo” (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya).

Photo: Prof. Gerard Misinzo (aliyesimama akiwa na kipazasauti) akifafanua namna ya kukishinda kirusi kinachosababisha ugonjwa wa Korona wakati akiwasilisha moja ya mada kuu katika Kongamano la Pili la Kisayansi lililofanyika ICE, SUA (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya).

Photo: Prof. Japhet Kashaigili, Mratibu wa Utafiti na Machapisho, DPRTC, SUA na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Kongamano la Pili la Kisayansi, SUA lililofanyika ICE, SUA akielezea jambo wakati wa Kongamano hilo (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya).

Maneno mazuri hata yanakosekana maana ni kama Tanzania ilihamia SUA. Ukigeuka huku Kongamano la Kisayansi, ukienda kule Maonesho ya Kumbukizi, na mdahalo wa kitaifa kuhusu “Teknolojia za Kilimo, Kuzalisha kwa tija na Ushindani wa Kibiashara nchini Tanzania Kuelekea Uchumi wa Kati Juu”.  Halafu siku inayofuatia mahafali ya aina yake hapa Chuoni yaliyofanyika mwezi wa tano. Mahafali hayo ya katikati ya mwaka ni nyongeza ya mahafali ambayo huwa yanafanyika SUA kuelekea mwishoni mwa kila mwaka.

Uratibu kupitia Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia (CSSH) ulikuwa mzuri katika kufikia mafanikio ya maonesho ya Kumbukizi ya Sokoine. Huko kwenye maonesho mambo yalikuwa motomoto. Kituo cha Kuthibiti Viumbe hai Waharibifu (SPMC), SUA walionesha, mara kufuga mende kwa matumizi mbalimbali, mara kunguni- waliokuwapo kwenye plastiki lililofunikwa, wakieleza namna ya kuwadhibiti. Halafu panya wanaotafuta watu waliofukiwa kwenye vifusi, ilifurahisha sana.

Picha: Prof. Samwel Kabote, Rasi wa Ndaki ya CSSH, SUA akiongea mbele ya vyombo ya habari wakati wa shughuli mojawapo ya Kumbukizi ya Sokoine ambapo yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wiki ya Kumbukizi ya Moringe Sokoine, 2021 (Picha, shukrani kwa Noel Kakunya).

Picha: Panya  aliyefundishwa kutumika katika kuokoa watu waliofukiwa na vifusi vya majengo yaliyoanguka akiwa amebebeshwa Kamera (Picha, shukrani kwa Francis Mwakatenya).

Picha: Panya aliyefundishwa kutumika katika kuokoa watu waliofukiwa na vifusi vya majengo yaliyoanguka akiwa amebebeshwa Kamera inayotumika kuonesha kilichofukiwa kwenye vifusi (Picha, shukrani kwa Francis Mwakatenya).

Kama vile haitoshi wanafunzi wanaosomea Ualimu katika Ndaki ya Solomoni Mahlangu ya Sayansi na Elimu (SMCoSE), SUA wanaeleza kisayansi kuwa tabaka la dunia linaloitwa Mantle ndilo huifanya dunia ikae katika mizania- yaani kukaa mahala pake katika muhimili wake bila kuegemea upande mmoja. Ikitokea kitu fulani kikameguka kutoka sehemu ya dunia na kuathiri mizania, Mantle ambayo ipo katika hali ya ujiuji husogea ndani kwa ndani ili kusaidia kutengeneza mizania.

Picha: Mfano wa umbo la ndani la dunia unaotumika kufundisha somo la Jiografia ukioneshwa katika banda la maonesha la SMCoSE, SUA (Picha, shukrani kwa Dk. Silvia Materu).

Sasa sijui ujiuji huo wa Mantle unapolipuka na kutoka nje kama Volkano ni katika kusadia dunia ikae kwa mizania? Hapa nilipitiwa kuuliza. Lakini wanafunzi hao wa Ualimu walisema Volcano inayolipuka kama siyo nyingi, ikimininika kwenye ardhi hutengeneza mbolea yenye rutuba nyingi maana ujiuji huo unaotoka ndani ya dunia huwa na madini mengi ya kulisha mimea.

Pongezi kwa wadau wote kwa kufanikisha.

Chereko!

Andiko hili linapatikana pia katika lugha ya Kingereza kwa kubonyeza  hapa au alama ya bendera ya Tanzania katika ukurasa wa mbele wa tovuti ya ICE.

Kwa maelezo zaidi kuhusu andiko hili tafadhali mwandikie Dk. Innocent H. Babili kwenye email: ibabili@sua.ac.tz