SUA yaimarisha Mafunzo ya Ufugaji wa Samaki aina ya Sato na Kambare

IMG 01301

Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kwa kushirikiana na Idara ya Sayansi ya Wanyama, Viumbehai Majini na Nyanda za Malisho (DAARS), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) iliendesha mafunzo ya aina mbalimbali ya ufugaji wa samaki kwa wajasiriamali, wafugaji na wataalam wa samaki katika kipindi cha mwaka 2019. Mafunzo hayo yaliyofanyika mara nne yalihusu ufugaji wa samaki aina ya sato, samaki aina ya kambare na uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya kambare[1].

IMG 01301

Picha: Washiriki wakifuatilia kwa makini mojawapo ya mafunzo ya ufugaji wa samaki yaliyofanyika ICE, SUA

Katika kipindi hicho, mafunzo ya ufugaji wa samaki aina ya sato yalifanyika mara mbili katika Taasisi ya ICE, SUA. Ya kwanza yalifanyika tarehe 06-09 Mei 2019 na ya mara ya pili yalifanyika tarehe 07-10 Octoba 2019. Mafunzo mengine ya ufugaji wa samaki yalifanyika kuanzia tarehe 30 Septemba hadi tarehe 05 Octoba 2019 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dodoma Tanzania. Mafunzo haya yalifanyika kwa ushirikiano kati ya SUA, UDOM na kampuni ya Mongolo Agri-Enterprises iliyoko Dodoma. Mafunzo haya yalihusu uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya Kambare. Mafunzo ya mara ya nne yalifanyika tarehe 16-20/12/2019 na yalifanyika ICE, SUA. Mafunzo haya yalihusu ufugaji wa samaki aina ya Kambare na uzalishaji wa vifaranga vyake (mbegu).

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya uzalishaji wa kambare yaliyofanyika Dodoma yalihusisha wajasiriamali (wamiliki wa Mongolo Agri-Enterprises) waliohudhuria mafunzo ya awali ya ufugaji wa samaki aina ya sato yaliyofanyika ICE, SUA mwezi mei 2019. Wamiliki hawa wa kampuni tayari wameanzisha shamba la ufugaji wa samaki aina ya sato wilayani Chamwino, Dodoma. Aidha, hivi karibuni wameanza ufugaji wa samaki aina ya kambare, mara tu baada ya kushiriki mafunzo husika. Vilevile, baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa kambare na uzalishaji wa vifaranga vya kambare, ambao ni wajasiriamali wadogo kutoka Kibaha, wameboresha shughuli zao za uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya kambare.

Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa hii andika kwa Dk. Innocent H. Babili: ibabili@sua.ac.tz

 

[1] Kuhusu Kambare: Kadiri ya Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza ya Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TUKI) inayopatikana kwenye mtandao www.elimuyetu.co.tz/ samaki aina ya Kambare anaitwa catfish kwa Kiingereza. Ifahamike kuwa Kiswahili sanifu cha samaki huyu ni Kambare na siyo Kambale kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watumiaji wa Kiswahili.